Mambo Ya Kufanya Ili Kuanza Na Kuendelea Kumiliki Majengo Ya Biashara Yenye Kipato Kizuri Kila Mwezi
Usipunguze kodi ya nyumba yako.Hii ni falsafa ambayo ninawashauri wawekezaji kwenye majengo ya kupangisha.
Hii ni kanuni ambayo inasaidia sana msimamizi wa majengo ya biashara kuendelea kuingiza kiasi kikubwa cha kipato endelevu kila mwezi.
Sababu Ya Kutopunguza Kiasi Cha Kodi.
Uwekezaji kwenye ardhi na majengo huathiriwa na udhibiti binafsi (personal control).
Udhibiti binafsi unaweza kuifanya nyumba ya biashara kuwa na thamani kubwa kuliko mwanzo ndani ya miezi michache tu.
Ukikubali kupunguza kiasi cha kodi ina maana umeishiwa mbinu za kuongeza thamani ya nyumba yako.
Hii ni hatari na haitakiwi kuvumiliwa. Kwenye ukarasa huu nimekuandalia njia za kuongeza thamani ya nyumba ya biashara ili kuepuka kupunguza kiasi cha kodi.
Mambo Yanayoongeza Thamani Ya Majengo Ya Biashara.
Moja.
Ukarabati na maboresho kwenye nyumba.
Ukarabati wa urembo wa nyumba. Huu unaweza kujumuisha;
✓ Kupaka rangi kwenye ukuta wa nyumba.
✓ Kuongeza kapeti mpya.
✓ Kuongeza tailizi kwenye sakafu.
✓ Kubadilisha mwonekano wa ukuta wa ndani ya nyumba, na kadhalika.
Kubadili muundo wa jengo (structural improvements). Ukarabati wa aina hii unaweza kuwa ni kama ifuatavyo;-
✓ Kuongeza idadi ya nyumba vya kulala.
✓ Kuongeza nafasi ya vyumba vya kulala.
✓ Kuongeza idadi ya jumla ya vyumba vinavyopangishika kwenye nyumba husika.
✓ Kuongeza madirisha yenye mvuto kwa wapangaji bora.
✓ Kuongeza ukubwa wa madirisha na milango kufuatana na mahitaji ya wapangaji wako.
Kila unapo ongeza thamani ya nyumba za biashara unaongezea thamani kwa wapangaji wako na thamani ya uwekezaji wako kwa ujumla.
Mbili.
Ongeza Kiasi Cha Kodi.
Hii inatakiwa kufanyika endapo hali ya soko mahalia ni nzuri. Unatakiwa kufahamu kiasi sahihi cha chini cha kodi na kiasi cha juu cha kodi kwenye mtaa nyumba yako ilipo.
Pia, ni muhimu sana kupangisha nyumba yako kwa wapangaji bora. Wapangaji bora watawavuta wapangaji bora kipindi kijacho.
Wapangaji bora ni wapangaji ambao wana hali nzuri ya uchumi na ni waaminifu kwenye ulipaji wa kodi ya nyumba.
Tatu.
Ongeza Huduma Kwenye Nyumba Yako.
Hapa tunapata makundi mawili (2) ya huduma. Huduma hizo ni kama ifuatavyo;-
(a) Huduma zisizo ingiza fedha moja kwa moja.
Huduma za aina hii ni kama vile;-
✓ Kuongeza uwanja mdogo wa michezo ya kifamilia kwenye nyumba ya familia nyingi.
✓ Kuongeza huduma za intaneti ya bure kwa wapangaji wako. Hii inaweza kuwa bure au ya kulipia.
✓ Kuongeza kituo cha kufanyia mazoezi ya viungo vya mwili. Hii inaweza kuwa ya bure au ya kulipia.
✓ Eneo la kuegesha vyombo vya moto vya wapangaji wako.
(b) Huduma zinazo ingiza fedha moja kwa moja ni kama vile;-
✓ Mgahawa mdogo wa chai na vitafunwa.
✓ Kuongeza chumba cha kuhifadhia bidhaa au vifaa mbalimbali (store room).
✓ Kuongeza huduma ya udobi kwenye nyumba yako ya familia nyingi.
✓ Kuongeza vyumba vya mikutano vya ukubwa tofauti tofauti.
✓ Kukodisha eneo la wazi kwa ajili ya michezo ya watoto, maonyesho ya sanaa na kadhalika.
✓ Kuongeza eneo la kuwalea watoto wadogo (daycare center) kwa nyumba za ofisi na nyumba za familia nyingi.
✓ Kuongeza huduma ya intaneti ya kulipia kwa wapangaji wenye matumizi makubwa ya vifurushi vya intaneti.
✓ Kuongeza kituo cha kufanyia mazoezi ya viungo baada ya kuona kuna uhitaji.
Nne.
Mikataba Ya Upangishaji Ya Muda Mrefu.
Majengo ya biashara huwa na thamani kubwa yanakuwa kwenye mikataba ya upangishaji ya muda mrefu.
Kwa kawaida majengo ya biashara yenye mikataba ya upangishaji ya muda mrefu huwa na thamani ya mara mbili au zaidi ya majengo hayo hayo yasipokuwa na wapangaji.
Ni vizuri kiasi cha kodi ya jengo la biashara kisikadiriwe kwa miaka zaidi ya miaka mitano ijayo
Hii ni kwa sababu ni vigumu sana kupata makadirio sahihi ya kiasi cha kodi kwa miaka sita, saba, na kuendelea.
Tano.
Lipe Jina Jengo Lako.
Hii huongeza upekee wa jengo lako la biashara. Ni njia mojawapo ya kujitofautisha na wawekezaji wengine wa karibu yako.
Sifa nzuri unazotoa kwenye huduma zako za majengo ya biashara linahusianishwa na jina la majengo yako ya biashara.
Mfano; unaweza kuliita jengo lako TUKUYU ACRES PLAZA, SUNNY ACRES PLAZA, MWANJELWA PLAZA, WEMA HOSTELS, na kadhalika.
Hakikisha jina linaandikwa na mchoraji mbunifu na mzoefu wa kuandika nembo.
Jina liwe linasomeka vizuri wakati wa usiku na mchana. Usiku ndio wakati mzuri wa kuwavuta wengi kupitia jina linalosomeka vizuri.
Sita.
Badili matumizi ya jengo lako la biashara.
Unatakiwa kubadili matumizi kutoka aina ya matumizi yenye kipato kidogo kwenda matumizi yanayoingiza kiasi kikubwa cha kipato endelevu.
Unaweza kubadili kiwanda kilicho kati kati ya mji au jiji na kuwa hoteli, ofisi, na kadhalika.
Unaweza kubadili vyumba vya ofisi kuwa ofisi kwa ajili ya kutolea huduma za afya kama vile duka kubwa la dawa (pharmacy).
Unaweza kubadili fremu za biashara kuwa vyumba vya kuishi. Unaweza kubadili vyumba vya kuishi kuwa fremu za biashara.
Lengo kuu la kubadili matumizi ya ardhi ni kuongeza kipato. Unaacha matumizi ambayo yanaingiza kiasi kidogo cha kodi na kuifanya nyumba iwe ya matumizi ambayo yanaingiza kiasi kikubwa cha kodi.
Haya ni baadhi ya mambo unayoweza kufanya ili kuepuka chanagamoto ya kupunguza kiasi cha kodi kwenye majengo ya biashara.
Mambo mengine ya kufanya ni kama ifuatavyo;-
✓ Kuongeza usalama wa nyumba kupitia geti imara, mfumo wa kengele za umeme (electrical alarm system), na milango na madirisha imara.
✓ Kupunguza gharama za usimamizi ikiwemo kuweka balbu za mwanga zinazotumia kiasi kidogo cha umeme.
✓ Bili zote kulipwa na wapangaji kwa kuwawekea mita za kuonyesha kiasi cha umeme na maji kinachotumika kwa wapangaji husika.
Ninaamini mambo haya yatakusaidia sana kuongeza thamani ya nyumba yako ya biashara. Hatimaye hutaweza kupunguza kiasi cha kodi.
Rafiki yako,
Aliko Musa.
WhatsApp; +255 752 413 711
Bofya Hapa Kujiunga Na Kundi La WhatsApp La ARDHI NA NYUMBA CLUB
https://chat.whatsapp.com/FeMEt5K2mYbKNYoPR8tRdX
Bofya Hapa Kujiunga Na Kundi La Telegram La ARDHI NA NYUMBA CLUB
https://t.me/joinchat/Ydwj2U9-NKtmMGY0
Bofya hapa, kisha andika barua pepe (email) yako ili uendelee kupata masomo mazuri ya ardhi na majengo.