Mambo 5 Ya Kuzingatia Wakati Wa Ujenzi Wa Nyumba Ya Kupangisha
Ni heri kununua nyumba ya kupangisha kuliko kujenga nyumba ya kupangisha. Lakini utatakiwa kununua kutoka kwa wauzaji waliohamasika sana. Kununua nyumba utatumia fedha kidogo kuliko kujenga nyumba.
Pia, huwezi kununua nyumba kwa bei nafuu kutoka kwa wauzaji wasiohamasika. Lakini kama umeamua kujenga wewe nyumba ya kupangisha. Hapo chini nimekuandalia mambo muhimu ya kuzingatia.
Moja.
Wastani wa gharama katika mtaa wako.
Ni kosa kujenga nyumba ya gharama kubwa kuzidi wawekezaji wengine kwenye mtaa wako. Hii ni muhimu sana kama viwanja vimepimwa na kuna utaratibu wa kutolewa vibali vya ujenzi.
Kujenga nyumba ya gharama kubwa kuliko wengine ni moja ya sababu ya kumiliki nyumba zinazoingiza kiasi kidogo cha kodi.
Bofya hapa kujiunga na mafunzo ya mwezi januari 2023...
https://chat.whatsapp.com/FeMEt5K2mYbKNYoPR8tRdX
Pili.
Mahitaji ya wapangaji.
Jenga nyumba kwa ajili ya wapangaji na sio nyumba kwa ajili yako. Unapochagua ramani nyumba hakikisha ni chaguo la wapangaji.
Mwekezaji anahangaika na ramani nzuri na kuvutia sana huku akisahau gharama atakazotumia. Kumiliki na kusimamia nyumba za kupangisha ni sawa na kumiliki biashara.
Je bidhaa zote za dukani kwa mwenye nyumba anajiuzia yeye mwenyewe?. Jibu ni hapana. Mwenye duka atanunua pepsi, fanta, malta na kadhalika. Hivi anajumua kwa sababu vimehitajika na wateja wake.
Kuna kasumba ya wawekezaji kujenga nyumba za kupangisha kwa mapenzi yao bila kuangalia mteja wao (mpangaji) anahitaji nini.
Tatu.
Beba majukumu ya usimamizi kwa 100%.
Mwenye nyumba anahusika moja kwa moja kuhakikisha anatumia gharama kidogo kujenga nyumba. Hakuna wa kumwachia majukumu hayo. Pengine timu yako inaweza kukusaidia kusimamia baadhi ya majukumu.
Lakini mwenye nyumba utahahakisha kila kitu unauliza kinapofikia. Jambo hili ni muhimu kufanyika hata kama wasimamizi wa ujenzi wa nyumba yako ni waaminifu.
Hii ni kwa sababu changamoto inaweza kutokea kwa sababu ya mapungufu yao. Mfano, kama msimamizi wa ujenzi ni mwaminifu kwenye masuala ya fedha na bajeti anaweza asiwe mwaminifu kwenye kutunza muda wa kufanya kazi.
Inawezekana msimamizi wao wa ujenzi yuko vizuri kwenye mahusiano na mafundi wengine lakini hawezi kufanyia kazi mahitaji ya vibarua wa ujenzi. Kama kweli unahitaji kupunguza changamoto nyingi za ujenzi wa nyumba yako ya kupangisha beba majukumu kwa 100%.
Nne.
Andika ripoti ya bajeti ya fedha, vifaa vya ujenzi na malighafi ya ujenzi.
Andaa ripoti ya makadirio ya gharama za ujenzi kabla ya kuanza kujenga. Hii inafanyika baada ya kuwa na ramani ya nyumba. Andika kila kitu kiwe kwenye mfumo wa nakala ngumu (hardcopy).
Gharama za mabati, nondo, saruji (cement) na kadhalika. Kila kitu kiwe kwenye karatasi.
Orodhesha vyanzo vyote vya mtaji fedha kwa ajili ya ujenzi wa nyumba yako ya kupangisha. Hii itakusaidia kuona sehemu isiyo na umuhimu kwa ajili wapangaji wako. Ni kosa kuanza ujenzi wakati hujui utatumia jumla ya shilingi ngapi.
Linganisha gharama za fundi na mchague fundi wa gharama nafuu. Chagua fundi wa mkono mzuri wa kujenga. Chagua fundi ambaye akijenga tofali zinabaki hazina mashimo mengi kwenye ukuta. Mafundi wengi hutumia kiasi kikubwa cha zege wakati wa kuchapia ukuta kwa sababu ya kupanga vibaya tofali.
Hakikisha tofali nzuri endapo unatumia tofali ndogo za kuchoma (bricks). Tofali ndogo za kuchoma kama zimepinda pinda zitapelekea matumizi makubwa ya saruji na mchanga.
Tofali mbaya za kuchoma zitaufanya ukuta uwe na vimilima na kupelekea rangi ya ukuta kukosa mvuto.
Hakikisha mwekezaji unatumia malighafi na vifaa vyenye ubora vya gharama nafuu. Kazi kwako kufanya utafiti kulingana na eneo unapoishi.
Tano.
Usanifu wa nyumba yako (Architectural design).
✓ Nyumba isiwe na kona nyingi. Nyumba yenye kona nyingi huongeza idadi ya tofali, nondo, mbao, mabati, madirisha na kadhalika.
✓ Nyumba iwe na vibaraza (verandahs) chache. Achana na kibaraza cha jikoni, nyuma ya nyumba, mbele ya nyumba na kadhalika. Kibaraza kimoja tu au viwili kwa ajili ya kuifanya nyumba iwe na mvuto kwa wapangaji.
✓ Idadi ya milango. Ondoa milango yote isiyo na ulazima kwenye ramani yako. Na baadhi ya milango inaweza kuweka pazia nzuri na nzito badala ya kuweka fremu ya mbao na mlango wa gharama. Mlango wa jikoni na milango mingine ya sebuleni.
✓ Nyumba iwe na umbo rahisi (simple shapes). Nyumba za maumbo ya pembe tatu, msonge, mviringo na kadhalika yana gharimu kiasi kikubwa sana cha fedha.
✓ Maumbo ya gharama nafuu ni mraba (square shapes) na umbo la mstatiri (rectangular shapes). Maumbo haya mawili yanakuwa na kona nne (4) tu za kuta za nje za nyumba yako.
✓ Ramani ya nyumba za familia moja, familia mbili, familia tatu na familia nne huingiza kiasi kidogo mno cha kodi ukilinganisha na ramani za nyumba zisizo za familia.
✓ Paa la nyumba ya ziada ya nyuzi 45 kati ya usawa wa tofali la juu la mwisho na bati hatumia kiasi kikubwa cha fedha ukilinganisha na paa fupi.
✓ Usimtumie gharama zisizo za lazima kwenye ujenzi wa paa la nyumba kwa sababu paa haiongezi thamani yoyote kwa wapangaji wako. Lakini kama ni ushauri wa kitaalamu kutoka kwa mkandarasi wako, hapo inalazimika kuingia gharama.
✓ Msingi wa nyumba. Msingi wa jamvi utumike pale tu ambapo ni ushauri wa mtaalamu wa ujenzi wa nyumba yako. Msingi wa mkanda hufaa zaidi kwenye nyumba za kupangisha kwa sababu ya kupunguza gharama za ujenzi.
✓ Changamoto ni kwamba wengi wana desturi ya kuchagua ramani za familia kwa sababu zao wenyewe. Pia, ni aina ya ramani za nyumba ambazo ni vigumu sana kupata wapangaji kwa wakati husika.
Bonyeza hapa kujiunga na mafunzo ya mwezi januari 2023...
https://chat.whatsapp.com/FeMEt5K2mYbKNYoPR8tRdX
Rafiki yako,
Aliko Musa.
Mbobezi wa majengo.
Whatsapp; +255 752 413 711