Makosa Saba (07) Yanayofanywa Na Wawekezaji Wanaoanza Kuwekeza Kwenye Ardhi Na Majengo
Usijifunze kwa makosa yako mwenyewe
Jinsi ya kuanza kuwekeza kwenye ardhi na nyumba imekuwa changamoto kwa wengi. Wasomaji wangu wanasema watafute kwanza mtaji, wakipata watanunua majengo ya kupangisha.
Wasomaji wengine wa mtandao wangu wa UWEKEZAJI MAJENGO wanasema hawana muda wa kujifunza uwekezaji kwenye majengo kwa kuwa wapo bize kutafuta mtaji fedha.
Kundi la tatu la wasomaji wa mtandao huu wanasema kuwa haiwezekani kuwekeza kwenye majengo kwa watu wa kawaida kama wao.
Haya ni baadhi ya maoni ambayo nimekuwa nikipata mara kadhaa kutoka kwa wafuatiliaji wa mtandao wa UWEKEZAJI MAJENGO.
Wakati sahihi wa kujifunza uwekezaji kwenye ardhi na majengo ni kama ifuatavyo;-
✓ Wakati na kabla ya kuchagua maeneo ya kuwekeza maisha yako yote.
✓ Baada ya kuchagua maeneo ambayo umebobea kwenye biashara na uwekezaji. Kama ardhi na majengo ni chaguo lako, unatakiwa kujifunza kwa bidii sana. Vilevile kama huwekezi kwenye ardhi na majengo, achana na kujifunza uwekezaji huu maisha yako yote.
Watu wengi humiliki nyumba mbili za kupangisha, duka la rejareja la bidhaa za nyumbani, hufuga kuku hamsini, na humiliki pikipiki moja au mbili kwa ajili ya kuingiza kipato.
Kwa utaratibu huu wa waliowengi ni vigumu sana kupata manufaa ya nyumba mbili za kupangisha unazomiliki.
Rudia sababu mbili nilizotaja hapo juu na uzifanyie kazi. Katika somo hili, nimekuandalia makosa saba (07) ambayo hufanywa na kundi kubwa la wawekezaji wanaonza kuwekeza kwenye ardhi na majengo.
Yafuatayo ni makosa saba (07) ya kuepuka kwenye ardhi na majengo;-
(i) Hawana Mtaji Wa Kutosha.
Wengi huanza kununua majengo bila kuwa na tathmini halisi ya makadirio ya gharama zote kutoka kununua, kukarabati hadi kuboresha jengo.
Hii hupelekea uhaba wa mtaji wa kuwekeza kwenye kununua au kukarabati jengo. Hatimaye hukata tamaa na kuanza kupambana na biashara nyingine.
Usifanye haraka kununua nyumba. Kuna maneno kuwa ardhi na majengo hupanda bei kila siku. Maneno haya yanayo ongelewa mtaani huwafanya wengi kununua nyumba kwa haraka bila kuwa na maarifa sahihi ya uwekezaji.
Unapununua hakikisha, unapata thamani ya nyumba au ardhi unayonunua.
Pia hakikisha, unanunua ardhi ghafi au nyumba zenye kasoro ili uweze kuziongezea thamani na kutengeneza faida nzuri.
(ii) Kupandisha Makadirio Ya Thamani Ya Ardhi Au Majengo Kuliko Uhalisia.
Wawekezaji wanaonza wanaona kila ardhi au jengo kina thamani kubwa. Huamini kuwa hakuna hasara kwenye uwekezaji wa ardhi na majengo.
Wakipata mtaji fedha kinachofuata ni kununua nyumba yoyote iliyo mbele yao. Hili ni kosa, hasa kama kweli umeamua kufikia uhuru wa kifedha kupitia uwekezaji wa ardhi na majengo.
Unatakiwa kufahamu thamani halisi ya jengo unalotaka kununua bila kushusha thamani au kupandisha kuliko kawaida.
(iii) Kununua Ardhi Au Jengo Bila Kujua Mmiliki Halali Wa Mali Husika.
Hutakiwi kununua ardhi au jengo ambalo hujui nani anayemiliki. Njia bora pekee ya kuhakikisha mmiliki halali wa ardhi au jengo unayotaka kununua ni kukagua hati miliki.
Usiambiwe maneno kuwa hii nyumba ni yangu, hivyo haina shida. Usilambe maneno matupu.
Unatakiwa kufahamu jinsi ya kupata hati miliki ya kwako ya umiliki wa ardhi au jengo unalotaka kununua.
Mambo haya unatakiwa ufahamu kabla ya kutoa pesa zako mfukoni. Fikiria umetafuta mtaji fedha kwa miaka fulani, halafu unapoteza mtaji huo siku moja.
(iv) Kushindwa Kukagua Ardhi Ghafi Au Jengo Unalonunua.
Unaponunua nyumba kwa mara ya kwanza unakuwa huna uzoefu na maarifa sahihi ya jinsi ya kuwekeza kwenye ardhi na majengo.
Kukagua ardhi au jengo kwa maongezi ya simu ni kosa, hasa kama ndio unaanza kuwekeza kwenye ardhi na majengo.
Unatakiwa kuwa na timu yako ya uwekezaji kwa ajili ya kukagua nyumba unayotaka kununua. Hakikisha kila kitu kwa macho yako mwenyewe, wahoji wanatimu wako kuhusu kasoro na mategemeo ya faida au kipato unachotegemea kutengeneza.
Hii itapunguza mshangao (surprise) baada ya kununua nyumba husika. Sio vyema kununua kwa maongezi ya simu kwa wawekezaji wanaonza.
Hii ni kwa sababu wawekezaji wanaonza kuwekeza kwenye ardhi na nyumba wanakuwa hawana mfumo bora wa kutafuta dili, kusimamia uwekezaji wao na kuongeza ufanisi kwenye uwekezaji wao.
Kukosa sifa hizi hupelekea wawekezaji walazimike kukagua kwa macho yao wenyewe huku wakiwa na timu yao ya uwekezaji kwenye ardhi na majengo.
(v) Kukarabati Nyumba Kabla Ya Kuwa Na Umiliki Halali (Hati Ya Miliki).
Wengi hutumia moto ulio ndani yao kuanza ukarabati na maboresho ya majengo ambayo hawana umiliki halali wa majengo yao.
Hili ni kosa ambalo huendelea kurithishwa miaka hadi miaka. Hutakiwi kufanya kosa aina hii ambalo walikuwa wanafanya wawekezaji wa kale kwenye ardhi na majengo.
Kitu cha kwanza kabisa unachotakiwa kuwa nacho ni vigezo, mbinu bora za mazungumzo na mtandao imara.
Pili; unatakiwa kuwa na hati miliki mapema sana mara baada ya kununua ardhi au jengo. Kisha unaendelea na hatua za kuendeleza ardhi au nyumba uliyonunua.
(vi) Kuwasikiliza Wamiliki Wa Nyumba Za Kuishi.
Steve McKnight kwenye kitabu chake kiitwacho From 0 to 130 properties in 3.5 years ametushirikisha utafiti kuwa 76% ya wawekezaji humiliki nyumba moja au mbili, 16% humiliki nyumba mbili au tatu na chini ya 8% humiliki nyumba za kupangisha za ya tatu.
Ni wachache sana kwenye jamii zetu ambao wamepata uhuru wa kifedha kupitia kuwekeza kwenye ardhi na majengo.
Sio kila mwenye nyumba anatakiwa akupe ushauri unaoweza kuufanyia kazi. Msikilize mwenye nyumba yeyote, lakini chunguza ushauri wake.
Kosa mojawapo la wanaonza kuwekeza kwenye ardhi na majengo ni kumsikiliza yeyote anayetaka kuwashauri.
Kibaya zaidi wawekezaji wengi hutoa ushauri kutokana na uzoefu kwenye nyumba moja wanayomiliki bila kujali uhalisia wa uwekezaji kwenye ardhi na majengo.
(vii) Kununua Nyumba Ya Kwanza Kwa Kutumia Mkopo Kwa 100%.
Kama ni nyumba kwa ajili ya kupangisha, hutakiwi kununua kwa kutumia mkopo wa 100% ya bei ya nyumba unayonunua.
Inapowezekana, tumia mtaji wako kwa 100% kununua nyumba yako ya kwanza. Kisha tumia mbinu ya B-R-R-R-R kunufaika zaidi na nyumba za kupangisha.
Muhimu; Jiunge na kundi maalum la mafunzo ya uwekezaji kwenye ardhi na nyumba. Nitumie ujumbe WhatsApp usemao " KUNDI LA MAFUNZO".
Mwandishi,
Aliko Musa
WhatsApp; +255 752 413 711
Huduma zote ninazotoa hizi hapa chini, Bofya na usome...
www.uwekezajimajengo.wordpress.com/huduma
KUPATA MASOMO KWA E-MAIL JIUNGE HAPA BURE
www.uwekezajimajengo.substack.com
KUJIUNGA NA KUNDI YA TELEGRAM
https://t.me/joinchat/Ydwj2U9-NKtmMGY0
HUDUMA NA VITABU VYA UWEKEZAJI KWENYE MAJENGO
https://wa.me/c/255752413711
Karibu sana