Makosa Kumi (10) Yanayofanywa Na Wanaotaka Kustaafu Mapema Kupitia Majengo Ya Kupangisha
Safari ya kustaafu mapema kupitia majengo ya kupangisha haitakuwa rahisi. Kama ingekuwa hivyo kila mtu angeweza kustaafu mapema kupitia majengo ya kupangisha.
Lakini kama tayari una KWANINI KUBWA YAKO unaweza kupata mafanikio makubwa mno kupitia majengo ya kupangisha hata kama una kila aina za changamoto.
Kama unataka ujenge nyumba moja au mbili ili zikusaidie kupata hela ya kununua mboga na unga kwa ajili ya familia yako. Hii makala haikuhusu, nenda tu kucheza bao au kufanya chochote ukipendacho.
Makala hii ninamwandikia mwajiriwa au mfanyabiashara ambaye anataka kujinasua na changamoto aliyonayo.
Hili ni somo maalumu kwa wale ambao wameajiriwa sehemu au wanamiliki biashara lakini kipato chao hakiwafanyi kuwa huru kufanya mambo mema na mambo makubwa wayatakayo.
Yafuatayo Ni Makosa Kumi Ambayo Hutakiwi Kufanya.
(01) Kutotengeneza Pesa Wakati Wa Kununua Nyumba.
Unatakiwa kujifunza jinsi ya kutengeneza pesa wakati wa kununua nyumba. Na pesa unayotakiwa kutengeneza ni 20% au zaidi ya bei ya nyumba (ikiwemo na gharama za ukarabati).
Mfano; unanunua nyumba kwa milioni saba na ukarabati unagharimu milioni moja tu. Basi hiyo nyumba ilitakiwa iuzwe milioni kumi. Hivyo wewe faida yako itakuwa milioni mbili.
Usiwe na mawazo ya kujiambia kwa kuwa huna shida, hauna haja ya kununua nyumba kwa bei nafuu. Ukweli ni kuwa shida unazo tena nyingi sana. Kama hauna shida, achana na uwekezaji kwenye majengo ya kupangisha.
Mwaajiriwa au mmiliki wa anakuwa kwenye mtego anaponunua nyumba ya kupangisha anaona kuwa uwekezaji huo kwake ni kitu cha nyongeza tu.
Ninaomba ubadili mtazamo rafiki yangu. Ukitaka kustaafu mapema kupitia majengo ya kupangisha ni muhimu mno kufuata kanuni hizi ndogondogo za uwekezaji kwenye majengo ya kupangisha.
Njia unazoweza kutengeneza pesa wakati wa kununua nyumba ni ukarabati wa nyumba, maboresho ya nyumba, muda wa kufanya malipo ya nyumba, kulipia cheti cha hati miliki ya kiserikali, bima ya majengo na njia zingine kufuatana na mazingira unayokutana nayo.
(02) Kununua Nyumba Ya Kwanza Ya Kupangisha Kwa Kutumia Mkopo.
Kwa mwaajiriwa au mmiliki wa biashara kwake kupewa mkopo inaweza isiwe chanagamoto sana ukilinganisha na mtu mwingine ambaye hana shughuli ya uhakika.
Lakini ni kosa kununua nyumba ya kwanza ya kupangisha kwa kutumia mkopo. Hii ni kwa sababu utatumia muda mrefu sana kumiliki nyumba ya pili.
Unatakiwa kununua/kujenga nyumba yako ya kwanza kwa kutumia pesa yako mwenyewe na usitumie kiasi kikubwa cha fedha kuzidi hali ya uchumi mahalia.
(03) Kukadiria Mapato Kuzidi Uhalisia.
Usiwe mwekezaji ambaye unakadiria kiasi cha kodi ambacho hakiwezekani kwenye mtaa wako. Hii itakusababia hasara kubwa kwa sababu utatumia kiasi kikubwa cha mtaji fedha na jumla ya kodi ya kila mwezi itakuwa kidogo sana.
Unatakiwa kuandaa jedwali la makadirio ya mapato kabla ya kununua/kujenga nyumba ya kupangisha. Kisha unaanza utekelezaji wa mradi wako.
(04) Kukadiria Gharama Za Usimamizi Kuliko Uhalisia.
Ni kosa kosa kuwa na bajeti ndogo ya gharama za ukarabati wa nyumba yako ya kupangisha. Unatakiwa kuwa na bajeti ya 05% hadi 10% kila mwaka katika kila nyumba.
Na gharama za usimamizi wa nyumba yako zinatakiwa kutokana na kodi nyumba kutoka kwa wapangaji wa nyumba yako.
Nyumba ambayo pesa za usimamizi zinatoka kwenye mshahara wako au faida ya biashara yako nyumba hiyo sio aseti tena. Nyumba hiyo sio kitega uchumi tena.
Ni nyumba inayokuingiza hasara. Itakuchelewesha kustaafu mapema kupitia majengo ya kupangisha. Hakikisha unakuwa na picha halisi ya jumla ya gharama za usimamizi wa nyumba yako ya kupangisha.
Unatakiwa kuandaa jedwali la makadirio ya gharama za usimamizi kabla ya kuanza ujenzi/kulipia nyumba.
(05) Kukarabati Nyumba Zaidi Ya Uhitaji.
Kila nyumba ina kiwango cha juu cha kufanya ukarabati wake. Nyumba A inaweza kuhitaji milioni moja ili iweze kuwa na thamani sawa na hali ya soko la mtaa husika.
Kinachoamua gharama za ukarabati wa nyumba ni bei uliyonunulia nyumba na hali ya soko ya mtaa husika.
Kwenye mtaa ambao nyumba za aina ya nyumba yako zina thamani ya milioni hamsini. Ni kosa kukarabati nyumba ili iwe na thamani zaidi ya milioni 80.
Waajiriwa wengi au wafanyabishara wengi humwaga kiasi kikubwa cha fedha kwenye nyumba za kupangisha wakiamini watapata wapangaji kwa urahisi zaidi.
Waajiriwa hutumia pesa kubwa kukarabati nyumba ili kuonyesha utofauti na nyumba za majirani zake. Hili ni kosa moja kwa moja.
Nyumba yako ya kupangisha ni biashara hiyo. Hakuna mashindano ya maonyesho kwenye nyumba za kupangisha. Nenda na uhalisia wa soko mahalia (soko la mtaa nyumba ilipo).
(06) Kuwaruhusu Wapangaji Kuishi Kwenye Nyumba Bila Kulipia Kodi.
Mfanyabiashara anapokuwa na nyumba za kupangisha anaweza kudharau na kuona kodi ya mpangaji sio kitu kwake.
Hivyo wapangaji wasumbufu anaachana nao na kuwahurumia waendelee kuishi bila kulipia kodi ya nyumba.
Hii itakupelekea kudorora kwa biashara yako ya nyumba za kupangisha na hata faida au mshahara wako utapungua kwa sababu sehemu ya faida/mshahara wako utatumika kukarabati na kuboresha nyumba.
Wapangaji wengine hulipia kodi kwa usumbufu sana kiasi kwamba unashindwa kupata muda wa kutosha wa kufanya biashara zako au mambo yako mengine. Hii nayo unatakiwa kutovumilia.
(07) Kuwa na Msimamizi Asiyefaa.
Msimamizi mahalia akiwa na tabia za hovyo hovyo ni rahisi sana kuongeza chanagamoto za nyumba za kupangisha. Utashindwa kupata kodi stahiki kwa sababu ya kuwa na msimamizi asiyefaa.
Ukiwa umeajiriwa au unamiliki biashara unatakiwa kupata msimamizi mahalia wa nyumba zako za kupangisha ambaye yupo makini na mwaminifu sana.
(08) Kuuza Nyumba Ya Kupangisha Kabla Ya Miaka Sita.
Hutakiwi kufanya papara kuuza nyumba kwa sababu zinakuongezea chanagamoto. Unatakiwa kujifunza jinsi ya kukabiliana na changamoto za nyumba za kupangisha.
Nyumba ya kupangisha inatakiwa ikuingizie kodi ya pango kwa zaidi ya miaka sita. Kwa miaka hii sita, unatakiwa kupata kodi kwa zaidi ya miezi kumi kila mwaka.
Na jumla ya gharama za ukarabati na usimamizi zisizidi asilimia 10 ya jumla ya kodi ya nyumba kwa kila mwaka.
(09) Kutokuwa Na Utamaduni Wa Kujifunza.
Mwaajiriwa unatakiwa kutenga muda kila siku kujifunza kuhusu nyumba za kupangisha. Hii itakupunguzia makosa mengi ambayo yanaweza kugharimu muda na fedha zako.
Kama kweli una nia ya dhati ya kustaafu mapema kupitia majengo ya kupangisha usiache kujifunza mara kwa mara.
Na njia pekee ya kujifunza mara kwa mara ni kuwa karibu na wabobezi na wenye taaluma za viwanja na nyumba.
Mimi ni moja ya hao, karibu sana uwe rafiki yangu tujadili kuhusu nyumba za kupangisha.
(10) Kutokuanza Kuwekeza.
Mwaajiriwa au mmiliki wa biashara ni mtu wa kujiahidi kila mwaka. Kila mwaka mpya unapoanza anajitahidi kujiapiza kuwa mwaka huu hautapita atakuwa anamiliki nyumba ya kupangisha.
Mwaka unapita hana hata kiwanja. Mwaka wa pili hana hata akiba ya kununua kiwanja. Mwaka wa tatu hana hata mshauri wa kumsukuma afikie malengo yake.
Mwaka wa nne anaanza kunyoshea vidole chanagamoto alizokutana nazo miaka iliyopita. Yeye ni mtu wa stori za kujifariji kwenye eneo lake la kazi.
Mtu wa aina hii ahasau kustaafu mapema kupitia majengo ya kupangisha.
Muhimu; Nitumie ujumbe " Kundi La UWEKEZAJI MAJENGO" ili kupata utaratibu wa kujiunga na kundi maalumu la mafunzo ya uwekezaji katika viwanja na nyumba.
Mwandishi,
Aliko Musa
WhatsApp; +255 752 413 711
Huduma zote ninazotoa hizi hapa chini, Bofya na usome...
www.uwekezajimajengo.wordpress.com/huduma
KUJIUNGA NA KUNDI YA TELEGRAM
https://t.me/joinchat/Ydwj2U9-NKtmMGY0
Karibu sana