Makubaliano kati ya mpangaji na mwenye nyumba ni jambo muhimu sana kufanyika.
Makubaliano kati ya watu hawa wawili ndio muongozo wa mahusiano, na jinsi ya kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazoweza kujitokeza kipindi ambacho mpangaji atakuwa katika nyumba ya mwenye nyumba.
Uwekezaji kwenye nyumba za kupangisha ni biashara ya mahusiano bora. Mwenye nyumba ambaye hana mahusiano bora na wapangaji hawezi kupiga hatua kubwa kwenye uwekezaji wake.
Mpangaji ni mteja wa mwekezaji mwenye nyumba za kupangisha. Mpangaji anatakiwa ajaliwe zaidi ya wateja wengine kwenye biashara.
Hii ni kwa sababu wapangaji ni wateja wako ambao wataendelea kununua huduma zako za makazi bora kwa miezi mingi.
Hivyo kuandaa makubaliano kati yako mwenye nyumba na mpangaji wako ni jambo la lazima.
Makubaliano yanaweza kuwa kwa njia ya mdomo au kwa njia ya maandishi. Lakini mimi nakushauri usifanye makubaliano kwa njia ya mdomo.
Makubaliano ya njia ya mdomo yatakugharimu mambo mengi. Makubaliano kwa njia ya mdomo yanaweza kusababisha hasara kubwa muda ambao changamoto zinatokea.
MFANO WA MKATABA; Kati Ya Mpangaji Na Mwenye Nyumba
Mkataba huu ni makubaliano umesainiwa TAREHE 05 MWEZI 08 MWAKA 2021 kati ya mpangaji anayeishi Sokomatola nyumba namba S/M/Str/0045 na mwenye nyumba ambaye ofisi zake zipo Mtaa wa Mwanjelwa sambamba na hospitali ya MARANATHA, Chumba namba 43, Mbeya Tanzania.
Mpangaji amepanga kutoka kwa mwenye nyumba na mwenye nyumba amempangisha mpangaji kwa kufuata sheria na kanuni zilizopo kwenye mkataba huu tangu tarehe ya kuanza kuishi 06-08-2021 hadi tarehe 06-11-2021 ambapo itakuwa ndiyo mwisho wa makubaliano haya.
Mpangaji atakuwa analipia tshs.50,000/= (ELFU HAMSINI TU) kwa mwezi kabla ya kufika saa 12 jioni ya kila tarehe 05 kwa kila mwezi. Mpangaji atatakiwa kulipia kupitia njia ya akaunti ya Benki A/C 62510003967 (Yenye Majina Aliko Musa Mwakabulufu).
Kodi ya nyumba au malipo yoyote hayatapokelewa kupitia njia ya aina nyingine mbali na njia iliyotajwa hapa.
Mpangaji atakuwa analipia elfu moja (tshs.1,000/=) kila siku baada ya kuchelewesha kulipa kodi.
Mpangaji ambaye atakuwa mwaminifu katika ulipaji wa kodi kwa miezi sita (06) mfululizo atapata punguzo ya kodi ya pango la nyumba la tshs.10,000/= au kufanyiwa ukarabati mdogo wenye thamani ya shilingi Elfu Kumi (10,000) tu.
Mpangaji anaruhusiwa kuishi na jamaa na ndugu zake watu wazima 2 na watoto 2 ambao majina ya ni kama ifuatavyo; Juma, Joseph, Simbachawene, na Kimambi.
Idadi ya wataoishi kwenye chumba hiki haitakiwi kuwa zaidi ya jumla watu watano (05). Mpangaji kuruhusu kukaa mtu mwingine tofauti (bila ruhusa ya mwenye nyumba) na waliorodheshwa hapa, mpangaji atastahili faini ya shilingi elfu hamsini (50,000) kama hakuna shida yoyote iliyojitokeza.
Kama shida itatokea baada ya kumkaribisha mgeni ambaye hajatambulishwa kwa mwenye nyumba au msimamizi wa nyumba, sheria itafuata mkondo wake.
Mpangaji ana wajibu wa kutunza mazingira ya ndani na nje ya nyumba kipindi chote cha kuishi katika nyumba hii.
Usafi au gharama za usafi wakati mpangaji anapoondoka utakuwa juu ya mpangaji mwenyewe.
Mifugo kama vile ng'ombe, mbuzi, nguruwe, kuku na bata itafugwa kwa uangalifu mkubwa. Hii ni kulinda usafi na ubora wa nyumba ya kupangisha.
Hakutakuwa na kodi ya ziada ya mifugo ya mpangaji, lakini uharibifu utakaotokana na mifugo hiyo utatakiwa kurekebishwa na mpangaji mwenyewe.
Ahadi yoyote na makubaliano yoyote yatakayo fanyika kwa mdomo bila kuingizwa kwenye mkataba huu, hayakuwa na maana na yatapuuzwa mara moja.
Mwenye nyumba atakuwa na haki ya kuhoji na kudai fidia ya mali zitazoharibiwa kutokana na sababu zifuatazo; uwizi, ukabaji, moto, uporaji, ukataji wa mabomba ya maji, umeme na vifaa vingine.
Hivyo basi, mpangaji ana wajibu wa kutunza nyumba na mali zote alizokabidhiwa wakati anahamia kwenye nyumba yako.
Mpangaji anashauriwa kulipia bima ya mpangaji kumkinga dhidi ya uharibifu unaoweza kujitokeza, hasa kama mpangaji ana jamaa au ndugu wengi.
Mwenye nyumba atakuwa na ruhusa ya kukagua nyumba yake kwa masaa na utaratibu unaoruhusiwa.
Mpangaji atatakiwa kuishi na jamaa zake kwa ustaarabu bila kuharibu furaha au kuwakera kwa kukusudia wapangaji au majirani zake.
Mpangaji ni lazima atoe taarifa haraka sana juu ya ukarabati wa dharura unaotakiwa kufanywa na mwenye nyumba.
Mpangaji atatakiwa kufanya ukarabati mdogo wenye thamani ya shilingi Elfu kumi ndani ya miezi sita, endapo utahitajika.
Malipo ya bili za maji, umeme, gesi ya kupikia na takataka yatakuwa yanalipwa na mpangaji mwenyewe.
Mpangaji atatakiwa kulipa ada ya usalama wa mali shilingi ELFU TANO (5,000) kila mwezi. Ambayo itakuwa inarejeshwa kwa mpangaji endapo hakuna uharibifu utakaojitokeza. Ada ya usalama itarejeshwa kwa mpangaji endapo;-
✓ Mkataba wa kuishi umeisha.
✓ Funguo zote amerudisha.
✓ Hakuna pesa anayodaiwa.
✓ Hakuna kasoro kwenye vifaa vyote vilivyomo ndani ya nyumba.
✓ Hakuna bili ya umeme, maji, takataka na nyingine anayodaiwa mpangaji anayeondoka.
Mkataba huu umekubaliwa mbele ya wapangaji wafutao;-
✓ Mpangaji A..................Aliko Musa
✓ Mpangaji B.................. Joseph Kidaru
✓ Mpangaji C.................. Asha Hassan
Mwenye nyumba au msimamizi wa nyumba..............Musa Mwaka.
Vifaa Na Samani Zilizopo (Appliances And Furnitures).
✓ Meza moja yenye urefu.....kimo.....na upana......
✓ Jokofu moja yenye uwezo wa.....WATTS.
✓ Viti....20 vya plastiki kampuni ya Jambo Plastics Ltd vyenye rangi ya njano...4, rangi nyeusi..5, na rangi nyekundu ...11.
✓ Meza moja ya kupikia jikoni kwa kutumia mtungi wa gesi yenye urefu....... Kimo....... na Upana.........
___________________________________
Mpangaji
TAREHE ____________________
Muhimu; Jiunge na kundi maalum la mafunzo ya uwekezaji kwenye ardhi na nyumba. Nitumie ujumbe WhatsApp usemao " KUNDI LA MAFUNZO".
Mwandishi,
Aliko Musa
WhatsApp; +255 752 413 711
Huduma zote ninazotoa hizi hapa chini, Bofya na usome...
www.uwekezajimajengo.wordpress.com/huduma
KUPATA MASOMO KWA E-MAIL JIUNGE HAPA BURE
www.uwekezajimajengo.substack.com
KUJIUNGA NA KUNDI YA TELEGRAM
https://t.me/joinchat/Ydwj2U9-NKtmMGY0
HUDUMA NA VITABU VYA UWEKEZAJI KWENYE MAJENGO
https://wa.me/c/255752413711
Karibu sana