Acha Mipango Ya Kujenga Nyumba Ya Kupangisha, Badala Yake Nunua Ikiwa Kuna Sababu Hizi
Somo hili ni maalumu kwa wawekezaji kwenye ardhi na majengo. Somo hili haliwahusu wanaotaka kumiliki nyumba za kuishi. Tafadhali zingatia hili.
Wawekezaji kwenye nyumba za kupangisha wana kasumba ya kujenga nyumba badala ya kununua nyumba za kupangisha.
Lengo kuu la kumiliki nyumba za kupangisha ni kutengeneza kiasi kikubwa cha kipato endelevu kwa kila mwezi.
Usifurahie umiliki wa majengo ambayo yatakosa wapangaji kwa miezi mingi. Furahia kumiliki malengo ambayo yanakuingizia kiasi kikubwa cha kipato endelevu cha kila mwezi.
Kwenye ukurasa huu nimekushirikisha faida na changamoto za kununua dhidi ya faida na changamoto za kujenga nyumba za kupangisha.
Faida Za Kujenga Nyumba Mpya Ya Kupangisha.
Moja.
Gharama ndogo za ukarabati na maboresho.
Kwa kawaida nyumba mpya hufanyiwa ukarabati wa kati kuanzia miaka 2 hadi miaka 3. Kwa kipindi cha miaka hii ya mwanzo, mwekezaji ataendelea kukusanya kodi bila kufanya ukarabati wa mara kwa mara.
Mbili.
Ramani Ya Kisasa (Ground floor plan).
Hili ni muhimu sana kufuatia eneo nyumba ilipo. Ramani ya nyumba ni sababu ya pili ambayo washindani wako hawawezi kushindana na uwekezaji wako.
Eneo la kwanza la kuwashinda washindani wako ni eneo ambapo nyumba ipo. Eneo la pili ni ramani ya nyumba.
Kwa sababu unajenga mpya, unakuwa na uhuru wa kumtumia msanifu majengo (structural engineer/architect) ambaye anaweza kukupa ladha uitakayo.
Tatu.
Mifumo Inayotunza Nishati (Energy-Saving System).
Mifumo ya sasa ya umeme imeboreshwa sana ukilinganisha na mifumo ya umeme ya miaka kumi na tano iliyopita.
Mifumo ya kupambana mazingira ya baridi kali na joto imeboreshwa sana ukilinganisha na mifumo ya miaka kumi iliyopita.
Kwa kuwa unajenga nyumba mpya, utapata nafasi nzuri ya kuchagua mifumo iliyoboreshwa.
Mifumo ya bomba za maji imeboreshwa ukilinganisha na mifumo ya bomba kwa miaka kumi na tano iliyopita.
Kwa sasa kuna mita za maji za kigitali. Mita hizi za maji ni rahisi kujifunza kuzisoma. Pia, unaweza kuchagua koki ya maji ambayo hutoa maji kidogo kidogo kulingana na mahitaji husika.
Hii itasaidia sana kupunguza kiasi cha bili za maji ya kila mwezi. Unahitaji kufanya kazi na mafundi wenye uzoefu mkubwa kwenye maeneo yao ya ubobezi.
Nne.
Njia Mpya Za Maji Na Takataka Za Halmashauri (Municipal water and sewage).
Ni rahisi kupata njia mpya zilizoongezwa na halmashauri husika unapojenga nyumba mpya kuliko kama ungenunua nyumba ya zamani.
Tano.
Usalama Wa Mazingira Na Kutokuwepo Na Madini Hatarishi.
Madini ya Zebaki na asbestosi huwa yanakuwa hayapo kwenye mazingira ya nyumba mpya hasa kama ni mtaa mpya.
Sita.
Nyumba Mpya Huvutia Wapangaji Bora.
Nyumba kuu kuu huwa inakosa mvuto kwa wapangaji bora ukilinganisha na nyumba mpya.
Changamoto Za Kujenga Nyumba Mpya Za Kupangisha.
Moja.
Hati Miliki Na Kibali Cha Ujenzi.
Ukiamua kujenga nyumba mpya utahitaji kiwanja. Kama kiwanja hakijapimwa, utahitaji kupima ingawa sio lazima kwa baadhi ya halmashauri.
Utahitaji kibali cha ujenzi kwa baadhi ya halmashauri ili kujenga nyumba mpya ya kupangisha.
Vitu hivi viwili vinaweza kukuchosha sana ukikutana na changamoto za kiutawala kwenye halmashauri husika.
Pia, utahitaji kupima udongo kulingana na aina ya jengo unalotaka kujenga. Vilevile utatakiwa kuandaa uwanja kwa ajili ya ujenzi wa nyumba mpya.
Mbili.
Maarifa Sahihi Ya Soko La Nyumba Za Kupangisha.
Unapojenga nyumba mpya kwa ajili ya kupangisha ni vigumu kuwa na uhakika kwa asilimia 100 endapo nyumba itakuwa na wapangaji bora kwa muendelezo.
Lakini ukinunua nyumba ya zamani, unaweza kutafuta nyumba ya kupangisha ambayo tayari ina wapangaji bora ndani yake.
Pia, unaweza kufanya tathimini ya historia ya upatikanaji wa wapangaji bora wa nyumba unayotaka kununua.
Tatu.
Muda Wa Kusubiri.
Unahitaji muda wa kutafuta kiwanja. Unahitaji muda wa kupima kiwanja. Unahitaji kufuatilia hati miliki kabla ya kuanza ujenzi wa nyumba mpya ya kupangisha.
Unahitaji kuwekeza muda kutafuta kona ya mtaa ambayo ina historia nzuri ya kuwa na wapangaji bora.
Unahitaji kusubiri kutoka siku ya kuanza ujenzi wa nyumba mpya hadi siku ya kuingiza wapangaji bora.
Nne.
Gharama za ujenzi miaka iliyopita ni kubwa ukilinganisha na mwaka huu.
Gharama za ujenzi mwaka 2021 mwezi februari zipo tofauti sana na mwaka 2022 mwezi Januari. Saruji imeongezeka bei, bati zimeongezeka bei na vinginevyo.
Tano.
Usimamizi wa ujenzi.
Unahitaji umakini na uangalifu wa kuwasimamia mafundi ujenzi. Mafundi wengi ni wasumbufu sana. Unaweza kuingia gharama zisizokuwa za lazima ikiwa utakosa umuhimu.
Sita.
Hofu Wakati Wa Ujenzi.
Hofu ya kuibiwa malighafi na vifaa vya ujenzi wa nyumba yako mpya. Hofu ya kutomudu gharama za ujenzi. Hofu ya kutoroka kwa mafundi ujenzi.
Faida Za Kununua Nyumba Ya Kupangisha.
Moja.
Nyumba za zamani huuzwa kwa gharama nafuu.
Kwa kawaida nyumba za zamani huuzwa bei nafuu ukilinganisha na jumla za gharama za ujenzi na bei ya kununulia nyumba mpya.
Mbili.
Muda mfupi wa kusubiri kuanza kupangisha.
Tatu.
Kumiliki nyumba ya zamani kwenye mtaa uliondelezwa.
Nne.
Unapata kupanga njia za kufanya ukarabati na maboresho bora kwenye nyumba unayonunua.
Tano.
Unaweza kununua nyumba kwa mkopo kutoka benki endapo nyumba ina kipato chanya cha kila mwezi.
Sita.
Kupata nafasi ya kuomba punguzo la bei. Unaweza kutengeneza zaidi ya 20% ya bei ya nyumba.
Changamoto Za Kununua Nyumba Ya Kupangisha.
Moja.
Kiasi kikubwa cha fedha za ukarabati na maboresho.
Mbili.
Nyumba kuwa na mifumo inayotumia kiasi kikubwa cha nishati ya umeme.
Tatu.
Kulipia gharama kubwa za bima ya majengo ukilinganisha na nyumba mpya.
Nne.
Wanunuzi kuingia kwenye ushindani mkubwa wakati wa kununua nyumba ya zamani.
Tano.
Kukosa ramani ya nyumba nzuri na inayoingiza kiasi kikubwa cha kodi.
Haya ni mambo ambayo unatakiwa kuzingatia kabla ya kufanya maamuzi ya kununua au kujenga nyumba mpya ya kupangisha.
Chagua kile ambacho kitakufanya utumie kiasi kidogo cha mtaji fedha. Kama hauna mtaji fedha ninapendekeza utafute nyumba ya kipato kizuri kisha tafuta mbia.
Muhimu; Lipia elfu tano (Tshs.5,000/=) ili kupata uchambuzi wa vitabu vya ardhi na nyumba, namna ya kuanza kuwekeza na ushauri. Kwa malipo haya utajifunza mwezi mmoja (siku 30).
Rafiki yako,
Aliko Musa.
Nitumie ujumbe usemao "ARDHI NA NYUMBA CLUB" ili ujiunge BURE kwenye kundi hili la WhatsApp na Telegram.
WhatsApp; +255 752 413 711